Breaking News
recent

PIUS MSEKWA ATOA SABABU YA CCM KUNG'ANG'ANIA SERIKALI MBILI


Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa
ametoboa siri ya chama hicho kung’ang’ania Muungano serikali mbili akisema hiyo ndiyo
sera yake pekee iliyopitishwa na wanachama wake wote kwa kura ya maoni.
Msekwa alieleza hayo katika mahojiano maalumu na wahariri wa gazeti hili
yaliyofanyika nyumbani kwake Oysterbay, Dar Es Salaam. Msekwa ambaye katika habari iliyochapishwa
na gazeti hili jana alieleza kuwa binafsi, hana tatizo na suala la idadi ya Serikali katika
Muungano, alisema kamwe hawezi kukishauri chama chake kukubaliana na mapendekezo ya
Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya muundo wa serikali tatu.
“Siwezi kuishauri CCM kukubali serikali tatu. Hili la Serikali mbili ni sera ya CCM, siyo tu sera
ya kawaida, bali hii ni sera pekee iliyopitishwa na wanachama wote kwa kura ya maoni,”
alisema Msekwa ambaye pia ni Spika mstaafu wa Bunge.
Alisema tofauti na sera hiyo ya serikali mbili, sera nyingine za chama hicho huanzia katika
ngazi ya Kamati Kuu, kujadiliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) na kupitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa. Msimamo ulikoanzia Kiini cha sera hiyo kutengenezewa utaratibu maalumu, kilitokana na sakata la Kundi la Wabunge 55 (G55), kuanzisha agenda ya kutaka Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano na
hatimaye Bunge kupitisha Azimio la kuanzisha serikali hiyo.
Msekwa ambaye wakati huo alikuwa Naibu Spika lakini akiongoza Bunge kutokana na
aliyekuwa Spika, Chifu Adam Sapi Mkwawa kuwa mgonjwa, alisema ushauri wa kurudi kwa
wanachama wa CCM kuwauliza wanataka serikali ngapi ulitolewa na Mwalimu Julius Nyerere.
Itakumbukwa kuwa hatua ya Bunge kupitisha azimio hilo la kuanzisha Serikali ya Tanganyika
ilimkera Mwalimu hadi akatunga kitabu, Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania
akiwashutumu aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela na aliyekuwa Katibu Mkuu wa (CCM),
Horace Kolimba. “Mwalimu alitueleza kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa, kuwa Bunge
limekwishapitisha azimio na likipitishwa ni lazima litekelezwe na Serikali. Alisema
mkikataa azimio la Bunge hivihivi mtaleta mgongano wa kikatiba, msiamue peke yenu,
nendeni kwa wanachama wote muwaulize ili uamuzi uwe wa wote,” alisema.
Alisema kutokana na ushauri huo, mwaka 1993 CCM iliandaa na kusimamia upigaji kura za siri
za maoni katika kila tawi, wanachama wakitakiwa kujadili na kuchagua kati ya serikali
moja, mbili au tatu. “Matokeo yalipofika katika Halmashauri Kuu,
ilionekana wanachama walio wengi katika matawi mengi walitaka serikali mbili, na hapo
ndipo ikapitishwa sera ya serikali mbili,”
Unknown

Unknown

No comments:

Powered by Blogger.