Wawekezaji
kutoka nje, wametajwa kugeuka mawakala wa kutorosha fedha nje ya uchumi wa Tanzania,
kiasi cha mabilioni ya Dola za Marekani, ambayo yakibadilishwa, yanafikia
matrilioni ya Shilingi.
|
Fedha hizo
zimekuwa zikiporwa nchini kutoka serikalini kwa maana ya kukwepa kodi na katika
jamii, kupitia ununuzi wa bidhaa nje ya nchi, ambazo thamani yake
huchakachuliwa kwa kuongezwa kinyume na thamani halisi.
Hayo yamo
katika Ripoti ya Shirika la Global Financial Integrity (GFI), iliyotolewa jana
(May 19,2014) mbele ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Rished Bade na Gavana wa
Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.
“Biashara
hii inayofanyika kwa kificho kwa kutumia mifumo ya kihasibu, imekuwa ikipora
serikali na jamii fedha zinazohitajika kwa ajili ya kukuza sekta binafsi,
ujenzi wa miundombinu na kutoa huduma muhimu.
“Tafsiri
yake, biashara hii imekuwa ikiondoa fursa za maendeleo, nafasi za ajira na lulu
ambazo zinapotea kiuchumi,” imeeleza ripoti hiyo.
“Zaidi ya
Dola za Marekani bilioni 8 (zaidi ya Sh trilioni 10) katika mzunguko wa fedha
zimehamishwa nje ya uchumi wa Tanzania isivyo halali kati ya 2002 na 2011,”
imeeleza ripoti hiyo.
Pia,
imefafanua kuwa Serikali ya Tanzania katika muda huo, imekuwa ikipoteza mapato
ya kodi ya wastani wa dola za Marekani milioni 248 kila mwaka katika biashara,
ambayo kodi hazikulipwa.
“Katika
mahesabu jumuishi ya mtaji ghafi uliohamishwa katika uchumi wa Tanzania isivyo
halali (cumulative growth illicit flows), kupitia biashara hii ni dola za
Marekani bilioni 18.73 kutoka 2001 na 2011, na sehemu kubwa ilihamishwa katika
miaka mitano ya mwisho ya muda huo,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu
wa taarifa hiyo, katika ununuzi kutoka nje, wawekezaji hao wamekuwa
wakishirikiana na wauzaji, kudanganya thamani ya bidhaa walizonunua kutoka nje
kuwa ni ya juu, kuliko thamani halisi.
Matokeo
yake, wawekezaji hutumia mwanya huo kuhamisha fedha nyingi za kigeni kwenda nje
ya nchi, kwa jina la kununua bidhaa za thamani kubwa, kumbe wamenunua bidhaa za
thamani ndogo na fedha nyingine inakuwa imetoroshwa nje ya nchi isivyo halali.
“Makadirio
ya fedha zilizohamishwa katika uchumi wa Tanzania kwa kupitia mfumo huu wa
kudanganya thamani ya ununuzi wa bidhaa kutoka nje, yanaonesha sehemu kubwa ya
fedha hizo zimehamishwa katika ununuzi wa mafuta ambayo yamesamehewa kodi
katika kampuni za madini.
“Ufafanuzi
wa hili ni kwamba, inaonekana kampuni za madini, zimekuwa zikichakachua kwa
kuongeza thamani ya gharama zao za ununuzi wa bidhaa na huduma kutoka nje, ili
kuhamisha mtaji isivyo halali,” imeeleza taarifa hiyo.
Sehemu
nyingine ambayo imetajwa kuwa uchochoro wa kutorosha fedha nje ya nchi, ni
miradi iliyo katika Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZ), ambayo imepewa msamaha
wa kodi (import duty) katika malighafi zitakazoagizwa kwa ajili ya kuzalisha
bidhaa za hapa nchini, pamoja na msamaha wa kutolipa kodi (corporate tax) kwa
miaka 10.
BOT, TRA na PAC
wanena Gavana wa Benki Kuu (BoT) , Profesa Benno Ndulu alisema ripoti hiyo ni
muhimu, kwa vile imewazindua macho juu ya udanganyifu, unaofanywa na
wafanyabiashara wa kutorosha fedha na kuingiza nchini fedha haramu.
"Tuchotakiwa
ni kufanya kazi kubaini namna kampuni hizi za kutoka nje zinavyotoa taarifa za
uongo ili watoroshe fedha hasa katika eneo la mafuta," alisema Ndulu.
Kamishna
Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Rished Bade alisema ripoti ya GFI itaifanya
mamlaka yake, kutafuta mbinu za kupambana na tatizo hilo la biashara zisizo na ankara
halali, kushamiri na kuifanya nchi kupoteza mabilioni ya fedha.
Alisema TRA
imeshangazwa na wawekezaji kutoka nje, kukwepa kodi kwa kutoa takwimu za uwongo
juu ya bidhaa wanazonunua huko ambazo wanasamehewa kodi na namna wanavyotumia
takwimu hizo za uwongo kuingiza fedha haramu nchini.
Alisema TRA
kwa sasa inahangaika ili kuingia kwenye mkataba mkubwa wa kimataifa, ambao
utaisaidia mamlaka hiyo kubaini udanganyifu huo kwani utawezesha mamlaka
kuwasiliana na bidhaa zinakoenda kuuzwa na zinakotoka kuingia nchini.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kabwe Zitto
alisema kuingizwa na kutolewa nchini kwa fedha haramu kunatokana na misamaha ya
kodi ambayo inatolewa kiholela na Serikali.
"Ripoti
imedhihirisha kuwa misamaha ya kodi kwa wawekezaji hawa kumetoa mianya ya
wawekezaji hawa kutoa takwimu za uwongo kuonesha kuwa wamenunua bidhaa hizo kwa
bei kubwa wakati ni uwongo," alisema Zitto.
Chanzo:- Habari Leo
No comments:
Post a Comment