Ramani ya baada kigamboni kujengwa... |
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema hayo juzi usiku wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2014/15.
Wakazi wa eneo hilo, wameshauriwa kuendelea kuwa wavumilivu na kutokubali kurubuniwa kwa kuuza maeneo yao kwa wajanja, ambao inaelezwa baada ya viwango vya fidia kutajwa, wamejitokeza wakitaka kununua ardhi kwa bei poa, baadaye wafidiwe.
“Itambuliwe kuwa viwango vya fidia katika Awamu ya Kwanza ya Mradi ni shilingi 35,000 kwa meta za mraba sawa na shilingi 141,645,000 kwa ekari moja.
“Hiki ni kiwango kwa mujibu wa sheria kulingana na soko na thamani ya ardhi itakavyokuwa katika mji mpya. Watu wanasema mimi ni wakala wa viwanja Kigamboni, mimi ni Waziri wa Ardhi,” alisema Profesa Tibaijuka aliyeomba aidhinishiwe bajeti ya Sh bilioni 88.8.
Aliwatoa wasiwasi watu wanaodhani kuwa mradi huo umeshindikana. Alisisitiza kwamba viwango vya fidia ni vizuri, kulingana na soko na thamani ya ardhi.
Aliwataka wananchi wa Kigamboni kuwa na uvumilivu na imani na mradi huo, na kuwashukuru kwa uvumilivu na ushirikiano wao wa kutambua azma ya Serikali ya kujenga Mji Mpya mwenye viwango.
“Jambo hili ni gumu na linachukua muda, lakini hatua iliyofikiwa si haba kwa zoezi lenyewe. Niondoe wasiwasi kwa wale ambao wanadhani kwamba kazi hii imeshindikana na hivyo tuondokane nayo.
“Mradi huu umetajwa kwa jina katika Ibara ya 60(b)(iv) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2010 ambayo inaahidi ‘Kuanzisha Mji Mpya wa Kisasa wa Kigamboni (Kigamboni New City.’
“Hii ni ishara tosha kuonesha wajibu wa Serikali katika kutoa kipaumbele kutekeleza kazi hii,” alisema Profesa Tibaijuka na kuongeza, “kwa hiyo, mimi nasonga mbele.”
Alisema ukosefu wa fedha umechelewesha mradi, lakini hata hivyo, wamekamilisha uandaaji wa rasimu ya muundo wa Wakala wa Uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni (KDA) na kuanzisha ofisi eneo la mradi.
Alisema Machi 2014, aliteuliwa Mtaalamu wa Fedha na sasa ameanza kazi, jambo linalotarajiwa kuongeza kasi ya kupata fedha za kutosha za utekelezaji wa mradi huo. Kuhusu fidia, alisema, “Naomba nirudie kwamba ili kulinda maslahi ya wananchi, viwango vya fidia vilivyopangwa ni endelevu na wakati ukifika umahiri na umuhimu wake utaonekana.”
Alisema tayari kuna wataalamu kutoka Serikali ya Watu wa China ambao wamewasili kwa nia ya kushirikiana na wataalamu wa ndani katika kupanga Mji Mpya wa Kigamboni na miji ya Lindi na Mtwara.
“Wizara ina imani kuwa utaratibu huu wa kupata fedha za kuendeleza Mji Mpya wa Kigamboni ukikamilika, mambo mengi ya mwanzo yatapungua na kasi ya utekelezaji wa mji huo itaongezeka,” alisema Profesa Tibaijuka.
Katika maoni yake, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, alitaka Serikali iwashirikishe wananchi wa Kigamboni katika kila hatua ya utekelezaji, ikiwa ni pamoja na suala la fidia.
“Kamati pia inaiagiza Serikali baada ya kuwepo kwa ucheleweshaji mkubwa katika utekelezaji wa Mradi wa Mji Mpya wa Kigamboni, ni wakati mwafaka sasa kubadili mkakati wa utekelezaji kwa kushirikisha wabia wengine na wakiwemo wananchi wa Kigamboni,” ilisema taarifa ya Kamati iliyosomwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM).
Nayo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ilihoji kama mpango huo umefuata sheria kwa kiwango gani, kwani kumekuwa na malalamiko mengi.
No comments:
Post a Comment