Breaking News
recent

MWIGULU ACHANGIWA FEDHA AGOMBEE URAIS 2015

Mwigulu Lameck Madelu Nchemba

Na Sharon Sauwa, Mwananchi


Dodoma. Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema ameanza kuchangiwa fedha na Watanzania wanaoishi ughaibuni ili zimsaidie iwapo ataamua kuwania urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu bungeni jana, Mwigulu alisema amesikia makundi mbalimbali, wakulima, wafugaji na wanafunzi wa elimu ya juu, walitoa tamko lao juu ya kumtaka kugombea nafasi ya urais.
“Wakulima na wafugaji walisema kuwa nikigombea watachangishana fedha za kampeni kwa kutambua mimi ni mtoto wa maskini na mimi ni maskini,”alisema na kuongeza;
“Wanafunzi wa elimu ya juu walisema kuwa wao watatembea kwa miguu kuhakikisha kuwa kura zinatosha. Kuzungusha fomu niende tu siko pekee yangu.”
Alisema na walimu pia baada ya kupata mishahara kwa wakati sasa wamemwomba kugombea nafasi hiyo ya juu kitaifa.
“Watanzania walioko nje ya nchi walisema wanachangishana na kimsingi wameshaanza kuchangishana ili kuhakikisha kwamba nagombea,” alisema na kuongeza,
“Mimi naendelea kusema ni vizuri watu kukutathmini kwa sababu jambo la urais si kujaza nafasi ni kazi watu wanakutuma uwafanyie na wewe uwajibike kwao na wala si jambo la kutaka tu.”
Alisema wanakutuma kuifanya kazi hiyo baada ya kupima changamoto walizonazo na kuona nani anaweza kufaa katika kuzitatua changamoto hizo.
“Sauti ikiwa kubwa hivyo ni jambo jema ambalo wanaona kuwa unaweza kufanya kazi hiyo vizuri. Naheshimu sana mawazo yao, lakini kwa sasa nataka niweke nguvu katika usimamiaji wa bajeti ya serikali, sera na miradi ya serikali,”alisema na kuongeza:
“Na naweka mkazo kwenye majukumu haya niliyopewa ya sasa. Na mimi huwa ni kawaida yangu jukumu lolote ninalopewa najitahidi kufanya kwa nguvu zote, kwa moyo wote ili Watanzania waweze kunufaika.”
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, alisema muda ukifika ataongea kuhusu kama anagombea urais ama la.
“Mimi niko pia katika chama kwa hiyo naheshimu miiko ya chama, taratibu za chama kwa hiyo chama kitakaporuhusu watu waanze harakati hizo ndiyo tutasema,”alisema.
Kuingia katika siasa
Alisema siasa ndiyo ilimchochea kusoma kwa bidii sana shuleni kwa sababu alivyokuwa shule ya msingi kazi aliyokuwa akiitambua ni ualimu na uanasiasa.
“Mbunge wa wakati ule alikuwa mwalimu na baadaye akawa waziri. Kwa hiyo nilijua ukitaka kuwa waziri ni lazima uwe mwalimu na baadaye waziri. Pia nilikuwa naona watu wanaoheshimika kijijini walikuwa ni walimu,” alisema.
Alisema hakuna mfanyakazi na kiongozi ambaye unaweza kumwona kijijini pale isipokuwa mwalimu na mbunge.
“Toka nikiwa kidato cha pili, cha tatu darasani kwangu walikuwa wakiniita Mbunge wa Iramba. Na nilipomaliza kidato cha nne nikaanza kuishi maisha halisi ya kiongozi kwa kuingia chipukizi na baadaye umoja vijana,”alisema.
Alisema mwaka 2000 alishiriki katika maandalizi ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na daftari la wapiga kura. Hata hivyo, mwaka 2005 niliponea chupuchupu kushiriki katika uchaguzi kwa kugombea ubunge kwa sababu nilikuwa bado sijamaliza masomo yangu ya shahada ya uzamili.
Makada kupewa onyo
Mwigulu alisema chama hakikutoa onyo kutokana na watu kutangaza urais, bali kilitoa onyo kutokana na mienendo.
“Kuita wajumbe kuwapa fedha, kutengeneza makundi ndani ya chama. Kutangaza si kosa bali ukiangalia kwenye maelekezo yaliyotolewa mambo yaliyotajwa ilikuwa ni kutoa fedha kwa wajumbe ni mambo ya rushwa,” alisema na kuongeza;
“Ni mambo ya maadili pale ama kuwaita wajumbe katika vikao ambavyo si rasmi. Mfano chama chetu hakina wajumbe wa mkutano mkuu katika ngazi ya wilaya yaani wajumbe wa mkutano mkuu hawana kikao katika ngazi ya wilaya wala mkoa.”
Alisema na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete alishawaambia mtu anayeita wajumbe wa mkutano mkuu kwenye ngazi ya kata ama wilaya ni kosa hakuna kikao kule.
“Kosa halikuwa ni kutangaza ila ni mienendo ya rushwa na kukigawa chama,”alisema.
Kuhusu iwapo maonyo hayo yamesaidia, Mwigulu alisema ilisaidia kwa sababu kiwango cha ugawaji na hekaheka kilikuwa cha juu.
“Kwa hiyo ingesababisha ilani ya uchaguzi isitekelezwe vizuri. Kwa sababu watekeleza ilani ndiyo walewale wengine wamo mle kwa hiyo chama kiliona kuwa wangeacha utekelezaji wa ilani na kurukaruka kwenye uchaguzi,” alisema na kuongeza;
“Kuanzia udiwani, ubunge si unaona hawa ndiyo watekeleza ilani wenyewe. Kama miaka mitano nyie mnazungumza mambo ya uchaguzi tu hamuwezi kutekeleza mambo ambayo Watanzania wanataka kuyaona kwa hiyo imesaidia.”
Maadili ya Viongozi wa Umma
Mwigulu alisema yeye anaamini katika sheria yenyewe iliyounda Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa watu kuelezea mali alizonazo.
“Uchukuaji wa hatua baada ya maelezo, ndiyo vitu vya msingi ambavyo vitafanya watu kuogopa, lakini kama kujaza fomu peke yake haitafanya watu wawe waadilifu,”alisema.
Alisema muundo wa serikali umejaa ngazi zote ambapo kila mahali kuna vyombo vya dola na hivyo uchukuaji wa hatua ndipo mahali ambapo pana legalega.
“Kuonyesha mifano ya hatua ambazo watu wamechukuliwa ndilo bado linakosekana kwa sababu kwa kila wilaya mfumo mzima wa ulinzi na usalama umekamilika.
Alisema kama taifa litavuka hatua ya kujaza fomu, watu wakijieleza na kuchukuliwa hatua maadili yatarejea.
Mwigulu wa kabla ya unaibu uwaziri
Mwigulu alisema akipewa jukumu analifanya kwa jitihada na juhudi zote.
“Nilivyokuwepo bungeni, nje ya chama nilikuwa nafanya kazi ya chama. Lakini sasa ninafanya kazi ya Taifa. Kwa hiyo nilivyokuwa nafanya kazi ndani ya chama nilikuwa nafanya kwa nguvu na bidii zote,”alisema na kuongeza;
“Na sasa hivi nikiwa serikalini nafanya kazi kwa bidii kwa nguvu na jitihada zote. Kwa hiyo inategemea namba unayocheza ukiwa kipa kazi yako ni kudaka ukiwa beki kazi yako itakuwa ni kuzuia na ukiwa mshambuliaji kazi yako ni kufunga.”
Mwigulu alisema, “Huwezi kupewa kazi ya beki ukaanza kudaka uwanjani kisa uliwahi kuwa kipa, utasababisha penalti kila wakati.”
Alisema ndiyo maana alipopewa kazi ya serikali anafanya kwa bidii na kwa nguvu.
Siri ya skafu
Mwigulu ambaye wakati wote hupenda kuvaa skafu shingoni yenye rangi za bendera ya Taifa, alisema yeye hupendelea kuvaa skafu hiyo kwa kuwa hiyo ndiyo nembo ya Taifa.
“Utakumbuka kuwa nchi yetu ilikuwa haina utambulisho ambao unaweza kumtambua huyu ni Mtanzania ama la. Lakini pia watu hawana viashiria vyovyote vya kizalendo. Kuna watu siku hizi hata wimbo wa Taifa hawauheshimu, kuna wengine hata kuimba hawawezi,”alisema na kuongeza;
“Sasa mimi nikaona kuwa naweza nikajitia-identify (nikajitambulisha) na kujivunia taifa langu kwa kuvaa skafu yenye rangi ya nchi yangu.”
Pia alisema kuwa imekuwa ikimsaidia kwa sababu watumishi wote wakiliombea taifa wanaombea kwa ishara ya bendera ya Taifa.
“Kwa kuwa na mimi ninayo hapa, mambo yangu yananyooka tu,”alisema.
Upinzani
Mwigulu alisema upinzani katika bara la Afrika unaangalia kwa kiasi kikubwa upungufu badala ya mbadala.
“Kwa hiyo ukiona kila mahali tunaziba mianya ya mapungufu ujue kuwa ndivyo hivyo upinzani unaona hauna maana na haujajipanga,”alisema.
Alisema akiwa katika nafasi hiyo serikalini kazi yake kubwa ni kuhakikisha kuwa hakuna mianya ya namna hiyo.
“Lakini pia nahimiza mabadiliko maana kiu ya wananchi wakati wote ni kuona mabadiliko katika utendaji. Ndiyo maana napigania kuhakikisha kuwa mabadiliko yanaonekana na ndiyo maana wakati wote kauli mbiu yangu ni kuwa mabadiliko ni vitendo,”alisema na kuongeza:
“Mabadiliko si vyama vya siasa ila mabadiliko ni vitendo na watu wakishaona vitendo, uwajibikaji. Kwa hiyo maisha yao yanabadilika kutokana na vitendo vya uwajibikaji,”alisema.
Miswada bungeni
Alipoulizwa kuhusu miswada inayokwenda katika Bunge la Novemba 4 mwaka huu, Mwigulu alisema kama watakubaliwa miswada wanayotarajia kupeleka bungeni ni ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), Utawala wa Kodi na Bajeti.
Muswada wa bajeti unalenga katika kuongeza nidhamu katika matumizi.
Serikali ya awamu ya nne
Alisema serikali ya awamu ya nne imeweka misingi yote ya taifa kuwa nchi ya kipato cha kati.
“Skeletoni yake ikijazwa nyama tu nchi hii itakuwa nchi ya kipato cha kati. Kwanza utaona kwenye elimu sekondari kila kata ambazo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa wanaoenda vyuoni,”alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo awamu nyingine ni kuzifanya sekondari hizo kufikia ubora wa viwango unaotakiwa. Sekondari za kidato cha tano na sita katika tarafa tutakapofikia kiwango cha ubora itakuwa na mchango mkubwa sana katika elimu,”alisema.
Alisema pia kwa kuzifikisha sekondari na vyuo katika ubora unaotakiwa, kutalifikisha Taifa katika kipato cha kati.
Alisema upatikanaji wa wahudumu wa kutosha, dawa na majengo bora katika zahanati za kata kutafanya Taifa kuwa na kipato cha kati.
“Hizo ni sekta moja lakini ukienda katika nishati sasa hivi tunafikia asilimia 35 na kuendelea ya upatikanaji wa umeme. Na hilo miye nalisimamia kwa nguvu zote kwasababu kila fedha inayopatikana kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini nahakikisha inaenda. Kwa sababu kila sekta inategemea sekta hii,”alisema.
Alisema ukienda katika sekta ya maji, barabara mambo yako hivyohivyo naamini haya kwa pamoja yataifanya nchi yetu kuwa katika kipato cha kati. “Utaona serikali ya awamu ya nne imeliweka taifa hili katika kipato cha kati. Lakini pia ukienda katika raslimali, wakati serikali ya awamu ya nne inaingia madarakani mapato yalikuwa karibu bilioni 59 kwa mwezi lakini hivi sasa tunapambana kupata trilioni moja kwa mwezi,”alisema.
Alisema na nchi itakavyoingia katika uchumi wa gesi kutakuwa na bajeti ambayo inajitegemea badala ya kutegemea misaada ya wahisani.
“Ndiyo maana nasisitiza kuhusu uwajibikaji na maadili na kufanya kazi kwa mazoea ili kulifikisha Taifa katika nchi ya kipato cha kati,”alisema na kuongeza;
“Kuwepo kwa uwajibikaji, maadili na mgawanyo sawa wa raslimali nchi yetu itakwenda kuwa ya kipato cha kati katika awamu inayofuata.”
CREDIT: MWANANCHI
Unknown

Unknown

No comments:

Powered by Blogger.