Israel imeapa kulipiza kisasi
dhidi ya kikundi cha wapiganaji wa Hamas wa Kipalestina wanaosemekana
kuwateka na kuwaua vijana watatu katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa
mto Jordan.
Miili ya vijana hao Naftali Frenkel, Gilad Shaar
na Eyal Yifrach ilionekana Jumatatu jioni, baada ya kupotea kwa zaidi
ya wiki mbili.Israel imefanya mashambulio ya anga zaidi ya 30 katika Ukanda wa Gaza usiku kucha.
Majeshi ya Israel pia yamesambaa katika mji wa Palestina wa Halhul. Miili ilipatikana chini ya kifusi cha miamba karibu na mji huo. Afisa mmoja wa Israel anasema inaonekana kuwa vijana hao watatu waliuawa kwa kupigwa risasi mara baada ya kutekwa kwao.
Israel imewataja watuhumiwa wawili wa utekaji wa vijana hao kuwa ni Ayoub al-Kawasma na Abu Aisheh. Jeshi la Israel limesema lilitegua milipuko iliyokuwa imetegwa wakati wa kuzivamia nyumba za watuhumiwa hao.
Askari wa Israel walitegua milipuko katika nyumba za watuhumiwa wawili wa Hamas. Picha zimeonyesha uharibifu mkubwa uliofanyika katika nyumba ya Abu Aisheh.
Mpalestina mmoja pia aliuawa baada ya kuwarushia kilipuzi wanajeshi wa Israel waliokuwa katika operesheni katika mji wa Jenin ulioko magharibi mwa mto Jordan, mapema Jumanne, limesema jeshi la Israel.
No comments:
Post a Comment