Breaking News
recent

WASSIRA AMTAKA TUNDU LISSU AOMBE RADHI MAASKOFU NA MASHEHE

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na Sera), Stephen Wassira ameshauri wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kurejea bungeni na kama maoni yao ni ya wananchi, wasubiri wakati wa kura za maoni.

Aidha, Wasira pia amemtaka msemaji wa Ukawa, Tundu Lissu kuwaomba radhi mashehe na maaskofu ambao ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kwa kudai ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wamekuwa wakihongwa chakula, chai na fedha katika nyumba za viongozi.

Alitoa maoni hayo jana kwenye mdahalo wa Tanzania Tuitakayo uliolenga kuangalia ‘Nani anataka kuwazuia Watanzania kupata Katiba Mpya,” akiwa sambamba na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Profesa Ibrahim Lipumba na Lissu.

Alisema kama Ukawa wanaungwa mkono na wananchi, ni vyema watumie nafasi hiyo kurejea bungeni na kujadili rasimu ndani ya Bunge na baadaye wasubiri wananchi waamue.

“Kama wanachokiamini Ukawa kuwa wako pamoja na wananchi, kwanini wanakwenda kwa wananchi kabla hawajamaliza kazi. Warejee bungeni tujadiliane na kumaliza kazi halafu wakatushitaki kwa wananchi, tuone Ukawa watapata ngapi…  kwanini tuandikie mate na wino upo?”

Aliongeza: “Kama ni muundo wa serikali mbili au tatu utajulikana bungeni.”

Wasira alisema Ukawa wanatakiwa kujua kuwa sheria inataka Katiba kuandikwa ndani ya Bunge na si sehemu nyingine na kushindwa kufanya hivyo ni kukwamisha mchakato huo ambao umefikia hatua ya tatu.

Alisema watu waliokataa kurudi bungeni ndio wanaowazuia Watanzania kupata Katiba mpya sababu Katiba haiwezi kuandikwa nje ya Bunge.

“Wanaokataa kwenda bungeni ndio wavurugaji, Katiba haiwezi kuandikwa Kibanda Maiti au Ubungo, inaandikwa ndani ya Bunge Maalumu.”

Awali, Lisu alisema kati ya wajumbe 201 walioteuliwa na Rais kama wajumbe wa Bunge, 169 ni wanachama wa CCM wakiwamo mashehe na maaskofu na wamekuwa wakihongwa katika nyumba za mawaziri.

Katika hatua nyingine, Wasira amewataka wanasiasa kuacha kusemea wananchi masuala ya mchakato wa Katiba kwa kuweka mawazo yao na kuwa CCM haipingi mawazo ya wananchi.

“Wanasiasa kutoka vyama vya upinzani wanadai kuwa tunapinga mawazo ya wananchi kama yaliyowekwa kwenye rasimu ya Katiba, lakini wamekuwa wakiweka mawazo yao kwa kisingizio kuwa ni mawazo ya wananchi."

Naye Profesa Lipumba, alisema rasimu inapaswa kuboreshwa na kujadiliwa kulingana na rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba na kutuhumu CCM kuwa ndio wanaovuruga mchakato kwa kutaka kupitisha mfumo wa serikali mbili.

Kwa upande wa Lissu alidai kuwa machakato wa Katiba umekuwa ukiendeshwa kwa kupendelea wajumbe wengi wa CCM. BONYEZA HAPA 

SOURCE: MDADISI BLOG
Unknown

Unknown

No comments:

Powered by Blogger.