MFUMO MBOVU WA ELIMU NA TATIZO LA AJIRA TANZANIA
Kwa miaka
michache iliyopita tatizo la ajira limeanza kushika kasi Tanzania na kwa miaka
michache ijayo litakuwa tatizo sugu kama hatua za makusudi hazitochukuliwa.
Tatizo hili kila mtu analiona na viongozi mbalimbali wamekuwa wakilizungumzia.
Ni kweli tatizo lipo na linaonekana, ila ni kweli kila anaeliona anafahamu
chanzo halisi cha tatizo hilo? Na je njia na ushauri unaotolewa na viongozi
mbalimbali kuhusiana na tatizo la ajira zinaweza kulimaliza ama kulipunguza
tatizo? Wahitimu waliokosa ajira wanashauriwa kujiajiri, je tuna uhakika
wameandaliwa kujiajiri?
Lazima tujue
kiini cha tatizo ili tuweze kukabiliana nalo sawa sawa. Chanzo kikubwa cha
tatizo la ajira ni mfumo wa elimu. Tukiangalia historia ya elimu Tanzania,
tulirithi mfumo wa elimu kutoka kwa wakoloni na mpaka sasa tunatumia mfumo huo
ukiwa umefanyiwa marekebisho ya hapa na pale. Lengo kubwa la elimu ya kikoloni lilikuwa
kuandaa wafanyakazi na wasaidizi wa wakoloni. Walilenga kupata wafanyakazi
wachache wenye elimu za juu ili kuwa wasimamizi na wafanyakazi wengine wenye
elimu za kati kuwa wasaidizi. Walilenga tupata wafanyakazi wa serikalini,
viwandani na watoa huduma kama walimu na madaktari. Leo ni miaka zaidi ya
hamsini imepita tangu tupate uhuru na bado elimu yetu ipo kwenye mlengo huo huo,
kuandaa wafanyakazi. Sio vibaya elimu kuandaa wafanyakazi, tatizo ni kazi zipo?
Unaandaa wafanyakazi una viwanda? Una uwezo wa kuwaajiri? Sekta binafsi zina
uwezo kiasi gani wa kuajiri? Ukiangalia kwa makini uwezo wa serikali na sekta
binafsi wa kuajiri ni mdogo ukilinganisha na idadi ya wafanyakazi wanaozalishwa
kila mwaka. Kwa kuwa uwezo wa kuajiri ni mdogo ushauri unaotolewa kwa wahitimu
ni waende wakajiajiri. Ni ushauri mzuri ila wataanzia wapi kujiajiri? Mfumo
mzima wa elimu kuanzia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu unamfundisha mwanafunzi
kuajiriwa, nyumbani wazazi na jamii wanamsisitiza mtoto asome kwa bidii afaulu
vizuri ili apate ajira nzuri. Hata mwalimu anaemfundisha anamwambia “ukienda
kazini utafanya hivi.” Kwa mazingira yote haya unakuja kumpa jibu rahisi kwamba
aende akajiajiri. Ni ngumu sana kwa mtu huyu kufunguka haraka kwa sababu mfumo
mzima wa elimu na maisha umeshamharibu. Inabidi kwanza abadili mtazamo ndipo
aweze kukabiliana na mazingira hayo mapya kwake, kitu ambacho kinawaumiza na
kuwavuruga wengi kisaikolojia.
Kwa maoni yangu ni
muhimu kubadili mfumo wa elimu, ni vyema tukaangalia ni nini changamoto zetu
kama taifa na kuangalia mfumo mzuri wa elimu utaoweza kututoa hapa tulipo. Tuwe
na mfumo ambao mwanafunzi aliemaliza kidato cha nne akapata daraja sifuri ana
kitu cha kufanya na sio anaishia kuonekana ni mjinga ama amefeli. Hiyo ni
kitaifa na kiserikali na nina uhakika mengi yameandikwa na kushauriwa ila
utekelezaji ndio tatizo kubwa. Kwa kuwa wanaotakiwa kutekeleza hawafanyi hivyo
haiwezi kuwa sababu ya mtu mmoja mmoja kushindwa kubadili hili. Kila mtu achukue
hatua, wafundishe watoto wako, washwawishi ndugu na jamaa zako kubadili mtizamo.
Ushauri mkubwa ninaoutoa hapa kwa wanafunzi walioko shuleni na vyuoni ni
wafikirie nje ya boksi, hayo unayofundishwa chuoni anza kufikiria unaweza
kuyatumia vipi kujiajiri, soma maandiko na vitabu mbalimbali vinavyoweza
kukusaidia kimaisha na kiuchumi. Usisubiri ukifika mtaani ndio uanze kuhangaika,
jua kabisa unasoma ila huku mtaani ajira hakuna. Angalia wenzako waliokutangulia
wengi bado wako mtaani wakihangaika kutafuta ajira mwaka mzima mpaka miwili.
Ukiwa umejiandaa inakuwa afadhali kuliko ukiwa hujajiandaa kabisa.
“Huwezi
kubadili maisha yako kama hutobadili mtazamo/fikra zako”
NINI MAONI YAKO?
Posted by BonifaceJr
No comments:
Post a Comment