Breaking News
recent
Elimu ya ujasiriamali msingi wa maendeleo kwa vijana

UHABA wa ajira za kudumu nchini unaweza kuangaliwa katika jicho la kipekee, huku sababu kubwa ikiwa ni ukosefu wa elimu ya ujasiriamali.
Lazima tukubaliane kwamba vijana ambao hawana ajira za kudumu wanashindwa kutumia vema fursa za kimaendeleo zilizopo.
Mkufunzi wa Elimu ya Watu Wazima mkoani Kilimanjaro, Celestine Magesa, anasema elimu ya ujasiriamali ikitumika vema tatizo la ajira nchini hususan kwa vijana linaweza kubaki historia.
Anasema umefika muda serikali kuangalia upya taasisi na vyuo vinavyotoa elimu ya ujasiriamali na kuwapatia mitaala bora, sanjari na kuwasaidia pale inapobidi.
“Serikali inatakiwa kusaidia taasisi mbalimbali zinazotoa elimu ya ujasiriamli ili kuweza kuwa na vijana wengi ambao tayari ni weledi na watashi katika utendaji kazi wao wa kila siku,” anasena Magesa.
Kwa mujibu wa Magesa, taasisi mbalimbali za utoaji wa elimu ya ujasiriamali zinatakiwa kujikita zaidi katika kuwawezesha vijana kutumia rasilimali zilizopo tofauti na kuwapatia elimu ya nadharia pekee.
Magesa ametoa kauli hiyo kwa vijana wakati akikagua Kituo cha Ujasiriamali cha Mwalimu Cristina Education Centre kilichopo katika Kata ya Mwika Kusini katika vijiji vya Lole, Maring’a, Msae na Kinyamvuo.
Anasema ujio wa kituo hicho kutaweza kusaidia vijana wengi katika maeneo hayo kutokana na ukweli kuwa maeneo hayo hayana chuo cha ujasiriamali mbali na chuo cha ufundi Veta, ambapo wadau wa elimu hudai ni gharama kubwa.
“Leo hii tutakuwa tumewawezesha vijana kuondokana na adha ikiwa kituo hiki kitawawezesha kupata elimu waliyoikosa kwa muda mrefu,” anasema Magesa.
Kwa upande wake mwalimu wa ujasiriamali kutoka Veta Kanda ya Kaskazini, Geroge Temu, anasema uwepo wa kituo cha Cristina kutawapunguzia mzigo watu ambao hutafuta elimu kwa gharama kubwa.
“Watu wengi wamekuwa wakitafuta elimu kwa gharama kubwa zaidi lakini uwepo wa kituo hiki ni dhahiri kuwa kila mtu ana uwezo wa kupata elimu hii ili kuweza kupambana na uhalisia wa maisha kama ilivyo hivi sasa,” anasema Temu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mwalimu Christina Education Centre, Geraldina Fabian, anasema imefika mahali somo la ujasiriamali liwe masikioni mwa walio wengi tofauti na dhana zilizopita.
Kwa mujibu wa Fabian, watu wengi wameshindwa kujikwamua kiuchumi kutokana na kukosa fursa za elimu mbadala.
Anasema kituo hicho kimegharimu zaidi ya sh milioni mianne na kuwa kitawasaidia wakazi wa Mwika Kaskazini na maeneo mengine katika kupata mafunzo ya ujasiriamali.
Hata hivyo kilio cha Fabian pamoja na serikali kuangalia jinsi ya kusaidia vituo kama hivyo ili viweze kuwa chachu ya maendeleo katika nyanja ya kuwainua vijana na si kuwa na vyuo vichache ambavyo ni gharama kumsomesha mwanafunzi.
“Serikali ingekuwa inasaidia vituo kama hivi… mwisho wa siku vijana wengi wangepata elimu ya ujasiriamali na wangeweza kuondokana na mfumo wa kufanya kazi za ndani na badala yake wangejiajiri,” anasema.
Ni vema serikali itenge maeneo maalumu kwa ajili ya vijana wenye nia ya kuondokana na umaskini sambamba na kuwaunga mkono.
Sekta binafsi mara nyingi ndizo zinakuwa chachu ya maendeleo lakini ni hali ya masikitiko kusema kuwa serikali imekuwa ikizisau taasisi hizi na hata kutotoa ushirikiano wowote hali inayozifanya zishindwe kusonga mbele.
Lengo kuu katika shughuli za ujasiriamali ni kujikita katika kila nyanja ili kila mtu au kijana kufanikiwa katika shughuli husika kama sanaa, kilimo, uchimbaji mdogomdogo, biashara na huduma nyinginezo.
Ili kuwawezesha vijana hao kupata elimu hiyo ya ujasiriamali, ni ukweli ulio dhahiri kuwa sekta hiyo inahitaji fedha ili iweze kujiendesha na kuihudumia jamii na kutoa mchango wake kama ilivyo hivi sasa.
Hali ya ukosefu wa fursa za ajira nchini Tanzania inazidi kukua siku hata siku na kuwakumba zaidi vijana wanaohodhi asilimia kubwa ya tegemeo katika nguvu kazi ya taifa kwa zaidi ya asilimia 65.
Vijana wanaopita katika mifumo ya kuwajenga kitaaluma na fani bado wanakuwa wahanga wakubwa wa kadhia hii ya ukosefu wa fursa za kuajiriwa wala kujiajiri kutokana na mfumo mzima wa elimu waliyopitia.
Changamoto zilizopo hivi sasa kwa vijana kuna haja ya kuangalia namna ya kubadilisha mtizamo wa vijana ili ushiriki wao katika mambo ya maendeleo uwe na tija.
Mfano, leo hii vijana wakiitwa kwenye semina ya kuwanufaisha wao bado kwa sehemu kubwa watataka walipwe.
Ni kweli kuwa vijana wengi hawana mitaji, vijana wanahitaji mafanikio ya haraka haraka, lakini pia kufuatia takwimu zilizopatikana kutoka katika maeneo ya kujitafutia maisha ni ni vigumu kujua idadi yao.
Kukosekana kwa njia muafaka katika uendeshaji wa baadhi ya vyuo vya elimu ya juu hapa nchi kumesababisha vijana kujiingiza katika migomo.
Hali hii ikiachwa iendelee kama serikali haitatekeleza mapendekezo ya wadau wa elimu ambayo ni njia sahihi ya kupunguza vurugu na migomo na maandamano katika vyuo vikuu nchini, vijana watashindwa kujikwamua.
Unknown

Unknown

No comments:

Powered by Blogger.