Exclusive:PROFESA MUKANDALA AZUNGUMZIA SAKATA LA NECTA
UAMUZI wa Serikali ya Tanzania kufuta matokeo ya kidato cha nne limeliweka Baraza la Mitihani (Neta) njia panda. Baraza hilo limejikuta katika wakati mgumu wakutekeleza uamuzi huo huku viongozi wakuu wa baraza hilo wakitishia kujiuzuru.
Taarifa za ndani kutoka Necta zinadai kwamba Katibu Mtendaji wa Necta Joyce Ndalichako pamoja na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Professa Rwekaza Mukandala wamegoma kufuta matokeo hayo badala yake wameonyesha nia ya kujiuzuru nafasi zao ndani ya Baraza hilo,kwa madai kwamba wanauhakika na kazi waliyoifanya na serikali ilishirikishwa kabla ya matokeo hayo kutoka.
Akizungumza na Habarimpya.com leo, Mwenyekiti wa Bodi wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) Profesa Rwekaza Mukandala alisema kwamba wamepokea uamuzi wa serikali na tayari wameshaamua cha kufanya.
“Ingawa mimi siyo msemaji wa Necta lakini nafahamu kinachoendelea, nanimeshatoa maoni yangu kwa Katibu Mtendaji Joyce Ndalichako,hivyo ni vyema ukamtafuta kwa sababu yeye ndiye msemaji na mwenye mamlaka yakutoa tamko la mwisho juu ya maamuzi ya Necta”alisema Profesa Mukandala na kuongeza:
"Ndalichako anafahamu cha kufanya juu ya uamuzi wa serikali kwa sababu anafahamu maoni ya bodi, na yeye ndiye mwenye mamlaka yote juu ya uamuzi huo wa serikali, mimi siwezi kusema chochote kwani nitakuwa naingilia utendaji wake wa kazi.
Hata hivyo Habarimpya.com ilipopiga hodi katika Ofisi za Katibu Mtendaji huyo ikabainika kwamba alikuwa kwenye vikao na kwamba hakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari, "Katibu Mtendaji yupo kwenye vikao, hawezi kuzungumza na mwandishi wa habari, labda mtafute kwenye simu yake ya mkononi"alisema mmoja wa wafanyakazi wa mapokezi. Hata hivyo alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa wakati wote.
No comments:
Post a Comment