Rais Obama akitangaza kubakia kwa wanajeshi 10,000 Afghanistan katika Ikulu ya White House Mei 27, 2014.
Rais Barack Obama ametangaza kuwa Marekani itaendelea kuwa na wanajeshi 10,000 nchini Afghanistan baada ya mwisho wa mwaka 2014.
Alitangaza kuwa Marekani kisha itaendelea kuwapunguza wanajeshi hao ili
kufikia mwaka 2016 kuwe kumebakia na wanajeshi wachache sana.
Rais Karzai amekuwa akipinga kila hatua au pendekezo linalotolewa na
maafisa katika utawala wake hasa kuhusiana na uwezekano wa kuendelea
kuwepo na wanajeshi wa Marekani nchini humo baada ya mwisho wa mwaka
huu.
Wakuu wake wa kijeshi, washauri wa maswala ya usalama na Mawaziri wake
wengi, wangalitia sahihi mapatano ya usalama na Marekani mwaka uliopita.
Lakini yeye, hata baada ya kuitisha mkutano wa wazee uliotazamiwa
kuidhinisha mapatano hayo alikiuka matarajio ya wengi na kusema kuwa
hatii sahihi mapatano hayo.
Wagombeaji wa Urais wawili waliosalia kwenye kinyanganyiro cha Urais
kuchukua nafasi yake Karzai wanaunga mkono mapatano ya usalama na
Marekani na hiyo ndiyo sababu Rais Obama ametoa tangazo lake kuhusu
wanajeshi watakaobakia nchini humo, ikiwa yamebakia majuma mawilli kabla
ya awamu ya mwisho ya upigaji kura nchini humo.
Hata hivyo kusita kwa Rais Karzai kutia sahihi mapatano hayo
kumeimarisha kampeni ya wale nchini Marekani wasiotaka kuendelea kuwepo
wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan.
Sasa wanajeshi watakaobakia Afghanistan watakuwepo kwa mwaka mmoja pekee
kabla ya kupunguza idadi hiyo kwa nusu halafu baadaye kupunguza hadi
sufuri ifikapo mwisho wa mwaka 2016.
Maoni ya wengi hapa ni kuwa ni heri wanajeshi wa Marekani waendelee kuwa nchini humu kwa muda mrefu zaidi.
Mapigano yametokea nchini humu mara kwa mara hivi kwamba kuwepo kwa
wanajeshi wa kigeni nchini kungetoa hakikisho zaidi kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment