Awali ndugu
huyo ambaye alikataa kutajwa gazetini, alisema kuwa kifo cha Gashaza ni pigo
kubwa kwa familia hiyo, lakini hawana cha kufanya zaidi ya kuachia Polisi
kufanya kazi yao.
Kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, Gashaza
aliajiriwa na mamlaka hiyo 2006 akiwa Mkaguzi Mkuu wa Mafuta ya Petroli. Mwaka
2013 Gashaza aliteuliwa kuitumikia Mamlaka hiyo katika cheo cha Meneja wa
Biashara kwenye Idara hiyo ya Petroli.
Taarifa hiyo
ilieleza kuwa mnamo Mei 15, mwaka huu Gashaza alisafiri kwenda Dodoma kwa
usafiri wa ndege akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ewura kwenye kikao cha Kamati
ya Bunge ya Bajeti.
"Baada
ya kikao hicho, alirejea jijini Dar es Salaam Jumamosi Mei 17, 2014 saa tatu
usiku. Asubuhi ya siku iliyofuata, tarehe 18 Mei 2014, uongozi wa Ewura ulipokea
taarifa za kushtua toka kwa familia yake kwamba Gashaza amefariki dunia,"
ilieleza taarifa hiyo.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo akizungumza wa mkutano na
waandishi Dar es Salaam jana. Picha na Salhim shao.
|
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, alisema Gashaza alikutwa amejinyonga
kwenye nyumba ya kulala wageni ya Mwangaza Lodge kwa kutumia tai
aliyoiunganisha na waya wa pazia na kuitundika kwenye nondo za dirisha la
chumba namba 113.
Kamanda
Kiondo alisema chanzo cha kifo chake hakijafahamika lakini inasadikiwa kuwa
siku ya Mei 17, aliwaeleza ndugu zake kuwa ana matatizo ya kiofisi ambayo hata
hivyo hakuyaweka wazi.
Sintofahamu
imeendelea kugubika kifo cha Gashaza na sasa imeelezwa kuwa alirudi kutoka
Dodoma akiwa amejawa hofu na kukosa amani.
Aidha kukiwa na utata wa kifo cha Meneja wa Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), imebainika kuwa tofauti ya takwimu kati ya
mamlaka hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), iliyotolewa kwenye Kamati ya
Bunge ya Bajeti ni Sh25 bilioni.
Meneja huyo,
Julius Gashaza alikuwa akihudhuria kikao kilichokuwa kikijadili tofauti hiyo
bungeni Dodoma na baadaye aliporudi Dar es Salaam akakutwa amejinyonga hotelini
huku ikielezwa kuwa alirudi akiwa amejawa hofu na kukosa amani.
Vyanzo vyetu
ndani ya kamati hiyo vimeeleza kuwa tofauti iliyobainika katika hesabu za
taasisi hizo za Serikali ni lita 11,755,161, ambazo zingeuzwa kwa bei ya sasa
ya petroli mkoani Dar es Salaam ya Sh2,200 zingepatikana Sh25.86 bilioni.
Kwa mujibu
wa vyanzo hivyo, takwimu za TRA zinaonyesha kuwa kati ya Julai 2013 hadi Machi
mwaka huu, kiasi cha mafuta kilichoingizwa nchini kilikuwa lita 2,189,240,000
wakati Ewura ilionyesha ni lita 2,177,484,839.
Hata hivyo,
baada ya utata huo na Kamati ya Bajeti chini ya Andrew Chenge kuitaka Serikali
itoe ufafanuzi wa tofauti hizo, Serikali iliwasilisha taarifa yake Jumapili
ikisema takwimu zote ni sawa.
Katika
ufafanuzi wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema uhakiki wa
takwimu hizo ulibaini kuwa zote zilikuwa ‘sahihi’ na kwamba tofauti iliyopo
inatokana na upimaji wa mafuta.
Nchemba
alikaririwa akisema TRA hupima mafuta kwenye meli mara inapoingia na kukadiria
kodi wakati Ewura hupima mafuta yanapopokewa kwenye matanki.
“Kwa kuwa
wakati mwingine meli hutumia muda mrefu tangu zinapoingia hadi zinapoteremsha
mafuta, sehemu ya mafuta ambayo TRA huhesabu kama yameingizwa katika mwezi
mmoja wakati Ewura hupata takwimu za kiasi cha baadhi ya mafuta hayo katika
mwezi unaofuata na hiyo ndiyo iliyosababisha kuwapo kwa tofauti hiyo ambayo
hata hivyo ni ndogo.”
Kulingana na
takwimu hizo, kiasi cha mafuta kilichoonyeshwa na TRA kilikuwa juu kuliko kile
kilichoonyeshwa na Ewura na haijajulikana iwapo kutofautiana huko kwa takwimu
kuliifanya Serikali kumweka kitimoto Gashaza.
Uchunguzi wa
Jeshi la Polisi.
Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Temeke, Engbert Kiondo alisema uchunguzi wa chanzo cha kifo
hicho unaendelea kwa kuangalia maeneo matatu.
Alisema
utajielekeza kubaini kama kulikuwa na mgogoro wowote wa kifamilia au iwapo
alikuwa na tatizo lolote kazini kwake kabla ya kifo chake na mazingira
kilipotokea kifo hicho na baada ya kujiridhisha watatoa taarifa kamili kwa
vyombo vya habari.
“Kuna
maswali mengi ya kujiuliza kwa nini hakutaka kulala nyumbani kwake usiku ule
badala yake akaamua kulala hotelini, tunafanya upelelezi kubaini nini hasa
kilimsukuma kujinyonga,” alisema.
Alisema pia
wanasubiri ripoti ya uchunguzi ya daktari ambayo wataitumia katika upelelezi
wao kubaini chanzo.
Alisema
polisi watachunguza kama Gashaza alijinyonga kweli au aliuawa na kutengenezewa
mazingira ya kujinyonga.
Utata Bungeni.
Wakati
inaelezwa kuwa kulikuwa na tofauti ya takwimu kati ya zile za TRA na Ewura
kuhusu kiwango cha mafuta kilichoingia kwenye soko, taarifa zaidi zimeeleza
kuwa katika kikao cha Kamati ya Bajeti, Gashaza hakuulizwa swali hata moja.
Mmoja wa
wajumbe wa kamati hiyo alisema marehemu hakuhojiwa labda kilichomfanya ajiue ni
hofu iliyotokana na mahojiano baina ya kamati hiyo na watendaji wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REA).
Alisema
kamati hiyo iliwaita viongozi wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Nishati na Madini
ili kuwahoji kwa nini Sh50 zilizoongezwa katika mafuta ya petroli na dizeli
hazikwenda REA?
Mjumbe huyo
alisema kati ya zaidi ya Sh100 bilioni zilizotakiwa kwenda Rea ni Sh17 bilioni
tu zilizopelekwa na fedha nyingine zilielekezwa kwenye matumizi mengine ambayo
hayakuidhinishwa na Bunge.
No comments:
Post a Comment