Hii habari nimeitoa amkatanzania.com nimeona niwashirikishe wadau wangu muweze kufunga katika akili zenu kwa kuchanganua mambo.
Leo naomba niwe mganga na mtabiri wako kwa dakika tano
tu, baada ya hapo uganga na utabiri wangu utakuwa umeisha. Ila kabla ya
kuendelea naomba nikiri mambo mawili; sijawahi kuwa mganga na sijawahi
kwenda kwa mganga. Na kwenye makala hii naposema neno mganga namaanisha
mganga wa jadi.
Ukijifunza jinsi waganga
wanavyofanya kazi utaelewa kwamba waganga ni wanasaikilojia wazuri sana.
Waganga humsikiliza mtu kwa muda mrefu, humdadisi na kumuuliza maswali
mengi sana mpaka wanagundua imani ya huyu mtu iko wapi. Baada ya
kugundua imani hiyo wanaitumia kumpatia tiba husika. Hii ndio sababu
kuwa wanasema mganga hajigangi kwa sababu hawezi kutumia saikolojia hii
kwake mwenyewe. Mganga anaweza kukuaminisha wewe kuwa tajiri wakati yeye
sio tajiri, ni saikolojia hii ndio inatumika hapo.
Sasa
leo natumia saikolojia ya waganga kukueleza kwa nini hutafanikiwa hata
kama una uchu kiasi gani wa mafanikio. Kuna tabia nyingi sana ambazo
watu wasiofanikiwa wanapenda sana kuwa nazo wakati watu waliofanikiwa
hawana kabisa. Naposema mafanikio simaanishi fedha tu, bali kuishi
maisha ambayo unayafurahia, yenye kuongeza thamani kwako na kwa
wanaokuzunguka. Kama hujazijua tabia hizi leo nitazungumzia tano tu, ila
zipo nyingi sana. Kama ukiendelea kuwa na tabia hizi utaendelea kuwa
msindikizaji katika safari hii ya maisha.
1. Kumsikiliza kila mtu.
Kama
kila anayekuambia kitu kuhusiana na unachofanya unamsikiliza
nakuhakikishia hutopiga hatua kubwa. Katika jambo lolote unalofanya kuna
watu watakutia moyo na kuna wengine watakukatisha tamaa. Wapo
watakaokwambia haiwezekani au huwezi. Tena wanaokwambia haiwezekani
watakupa mpaka mifano ya walioshindwa. Kama unataka kufikia mafanikio
makubwa acha kuwasikiliza watu wanaokukatisha tamaa, chagua ni kitu gani
unatafanya na anza kukifanyia kazi mpaka ufikie mafanikio yako.
2. Unafanya kile ambacho kila mtu anafanya.
Huwezi
kuamini ila iko hivi, mafanikio makubwa yanakuja pale ambapo unakwenda
hatua ya ziada. Kwenye kila unachofanya kuna hatua ya ziada ambapo kama
ukienda hatua hiyo utafikia mafanikioa makubwa sana. Kama unaamka
asubuhi, unakwenda kazini, unafanya kazi ulizopangiwa, jioni unarudi
nyumbani, unalala na kesho unarudia tena huo mzunguko sahau kuhusu
mafanikio makubwa. Kama unafanya biashara kama kila mtu anavyofanya kwa
mtindo huo huo na mbinu hizo hizo ambazo kila mtu anayefanya biashara
hiyo anatumia unasogeza siku tu. Kama unataka kufikia mafanikio makubwa
NENDA HATUA YA ZIADA. Kama unaishi maisha ya bwana mike utasubiri sana na hutofikia mafanikio makubwa.
3. Unatumia muda hovyo.
Poteza
milioni mia moja, unaweza kuzitengeneza tena baada ya muda fulani,
poteza sekunde moja ndio umeisahau kabisa. Hakuna kitu chenye thamani
zaidi ya muda, lakini ndio tunautumia kizembe kuliko kitu chochote kile.
Ili uweze kufikia mafanikio makubwa lazima uweze kuwa na matumizi
mazuri ya muda wako. Tunaishi kwenye dunia yenye kelele nyingi, kuna
vyombo vya habari, simu, email, mitandao ya kijamii na maongezi mengine
yanayokusubiri wewe kila siku. Usipokuwa makini unaweza kuona unakwenda
na wakati kumbe unakwenda nje ya mstari wa mafanikio.
4. Unapenda majibu ya haraka.
Sijui
ni kitu gani kimeharibu dunia kwa sasa ila kizazi cha sasa kinapendelea
majibu ya haraka kuliko vizazi vivlivyopita. Unataka uanze biashara leo
na mwezi ujao uwe umetengeneza faida mara mbili ya mtaji!! Yaani
unataka upande mchungwa leo na wiki ijayo uanze kula machungwa. Hakuna
kitu kama hicho ndugu yangu, mambo mazuri yanahitaji subira na
yanahitaji uvumilivu. Usidanganyike na kelele unazopigiwa na watu kwamba
fanya hivi utafikia mafanikio ya haraka, hayo ni matangazo ili
kufaidisha biashara zao. Huwa napenda kutumia mfano huu mara kwa mara, huwezi kuwachukua wanawake tisa ukawabebesha ujauzito mmoja ndani mwezi mmoja wakatoa mtoto, kama unatafuta njia ya mkato ya kufikia mafanikio unaweza kuyapata ila hutofika mbali.
5. Una matumizi mabovu ya fedha zako.
Hili
nalo linatabia ya kushangaza sana. Ukiangalia kwa makini, waliofanikiwa
kifedha wana matumizi tofauti kabisa na wale wanaolalamika kutokuwa na
fedha kila siku. Wakati wale wenye fedha nyingi wakitafuta sehemu za
uwekezaji, wale wanaozipata kidogo wanatafuta viwanja vya kuzitumbua.
Hata kama unapata fedha kidogo kiasi gani ni lazima uwe na kiwango
ambacho uaweka pembeni. Jilipe wewe kwanza kwenye kila kipato unachopata
na hii itakusaidia kuweza kuwa na maisha yasiyo na hofu juu ya fedha.
Kujua zaidi jinsi ya kujilipa wewe kwanza soma makala hii unamlipa kila mtu kasoro huyu mmoja wa muhimu.
Hizi
ni baadhi tu ya tabia ambazo zitakuchelewesa au zitakuzuia kabisa wewe
kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Kila mwezi tunajadili
tabia moja ndani ya KISIMA CHA MAARIFA, kama umechodhwa na tabia za aina hii karibu kwenye KISIMA ili uweze kujenga mwelekeo mpya wa maisha yako.
Unknown
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment