Kwa ulimwengu wa sasa, ajira zimekuwa ngumu mno na pia
zimekuwa na usumbufu mwingi. Watu wengi wanatafuta kazi na nafasi za
kazi ni chache. Hata walio makazini nao hawazifurahii kazi kama zamani, sasa hivi mazingira ya kazi yamekuwa magumu, maisha magumu na mishahara haitoshi.
Kutokana na matatizo haya kimbilio pekee limekuwa ni kujiajiri. Ambao
wanatafuta kazi na hawapati inawalazimu kuanza kuwa na mawazo ya
kujiajiri. Waioajiriwa nao wanawaza kujiajiri ili kuondokana na
manyanyaso ya kwenye ajira.
Hata wewe una wazo hilo la kujiajiri ili na wewe uweze kuyatawala
maisha yako. Ama umeshajiajiri ila bado mambo hayaendi kama ulivyodhani!
Ukiwaangalia waliojiajiri ni wachache wenye mafanikio makubwa. Wengi
wanaendesha tu maisha yao kwa kujiajiri kwao na wengine mambo yanazidi
kuwa mabaya hata baada ya kujiajiri. Ni
tatizo gani linatokea kwa hawa waliojiajiri wachache kupata mafanikio
makubwa na wengi kuishia kusota? Kuna tabia moja ambayo watu wengi
wanayo na hiyo ndio inayofanya watu washindwe kufanikiwa wanapojiajiri.
Duniani kuna makundi mawili ya watu, kuna ambao wanaweza kupanga na
kufanya kitu na kuna ambao wanaweza kufanya vizuri ila mpaka waambiwe
wafanye.
Kujua wewe uko kundi lipi, tafakari maisha yako kwa muda na uangalie ni
mambo gani unayoyafanya vizuri na unayopendelea kufanya. Yale uliypanga
mwenyewe ama yale uliyopangiwa kufanya? Jiulize ni kitu gani
kinakufanya uamke asubuhi na mapema? Ni kwa sababu hutakiwi kuchelewa
kazini au kwa sababu unaamka kuianza siku yako na kuifurahia?
Wanaoweza kufanya mambo yao wenyewe bila kuambiwa ni sehemu ndogo sana
ya jamii na hawa ndio wanaofanikiwa kwenye ajira na hata nje ya ajira.
Wanaokuwa wafanyakazi bora na wanaopandishwa vyeo ni wanaofanya tofauti
na wengine.
Wanaosubiri kuambiwa cha kufanya ni sehemu kubwa ya jamii na wengi
wanaishia kuwa wafanyakazi wa kawaida na hata wakijaribu kujiajiri mambo
yanazidi kuwa magumu. Kama wewe huwa
unafanya jambo baada ya kuambiwa ufanye basi usikurupuke kujiajiri. Anza
kujenga tabia ya kupanga na kufanya mambo yako mwenyewe bila hata ya
kuambiwa. Kama umeajiriwa na unayajua majukumu yako basi wewe fanya kwa
ufanisi na ubunifu mkubwa. Usiishie tu kufanya vile unavyoambiwa, nenda
mbele na ongeza thamani zaidi. Kufanya hivyo kutakuongezea utaalamu na
pia kutakupatia tabia ya kuweza kujiajiri. Ili uweze kufanya zaidi na
kwa utofauti ni lazima utumie uwezo na vipaji vyako ulivyonavyo. Kila
mtu ni mbunifu hivyo hutokosa cha kufanya.
No comments:
Post a Comment