Unakutana na rafiki yako ambae mlipotezana miaka mitano au hata kumi iliyopita. Katika kuzungumza kuhusu maisha anakwambia yeye ana kazi au biashara inayolipa sana, ana nyumba mbili, magari matatu na mashamba. Ukijifikiria wewe huna kazi au biashara ya kueleweka, bado unaishi kwenye nyumba ya kupanga na usafiri wako ni daladala. Unajisikiaje baada ya kupata picha hii ya mwenzako?
Mbaya zaidi unakuta mtu huyo mlikuwa mnafaulu sawa darasani na hata wakati mwingine ulikuwa unafaulu zaidi yake. Unapata hasira na kujiona wewe umeshapoteza maisha! Hiki ndicho kinachotokea kwa watu wengi.
Kosa kubwa unalofanya kwenye maisha yako kila siku ni kujilinganisha na wengine, kosa hili ni baya sana na linakugharimu sana kwenye maisha yako. Unaweza kusema kujilinganisha na wengine kunakupa wivu wa maendeleo au kunakufanya ukazane zaidi, huo sio ukweli hata kidogo. Kujilinganisha na wengine na hasa pale wanapokuwa wamefanikiwa kushinda wewe ndio unazidi kujirudisha nyuma. Unajisikia vibaya sana kuona mtu uliecheza nae utotoni ana mafanikio mara mia ya uliyonayo wewe. Hapa ndipo unapoanza kuona labda wewe una kisirani na yeye ana bahati au alibebwa.
Kila mtu ni wa pekee
Dunia ina watu zaidi ya bilioni saba, lakini kati ya watu hao hakuna watu wawili wanaofanana kwa kila kitu, hata mapacha hawana ufanano wa asilimia 100. Wewe ni wa pekee, una uwezo mkubwa na vipaji vya kipekee. Hakuna mtu yeyote duniani anayeweza kufanya vitu fulani kama unavyoweza kufanya wewe.
Pamoja na kwamba kila mtu ni wa pekee, tumetengenezwa kuamini kwamba wote tuko sawa na mwishowe tunaamini inabidi tufanikiwe kwa usawa. Unakwenda shule ya chekechea na wenzako, baadae mnakwenda shule ya msingi, baadae wachache mnaendelea na sekondari mpaka hata vyuo mbalimbali. Katika wakati wote huu unafikiri wote mko sawa, mna malengo sawa ya kufaulu na kuwa na maisha mazuri. Ila baada ya kila mtu kutawanyika ndipo mambo yanapoanza kuwa mazuri.
Kila mtu anasafiri kwenye njia yake binafsi.
Tatizo la kujilinganisha linaanza pale unapofikiri mlikuwa kwenye niia moja ya safari kwa sababu mlianza pamoja. Hapa ndipo unapochelewa na kuachwa nyuma. Kila mtu anasafiri kwenye njia yake binafsi. Kuna ambao watafanya kazi na kufanikiwa sana, kuna ambao watafanya biashara na kufanikiwa mno. Pia kuna wengine watafanya kazi za utumishi na kuwa na maisha mazuri sana. Unapojaribu kujilinganisha na watu hawa ambao wako kwenye njia tofauti hujitendei haki wewe mwenyewe.
Kama hujafanikiwa kama wenzako walivyofanikiwa huenda hujajua ni kitu gani unachofanya kwenye maisha yako. Huenda hujajua ni kitu gani cha kipekee unachoweza kufanya na ukafanikiwa sana. Na kwa asilimia kubwa huenda unaiga maisha ya watu wengine.
Jilinganishe na wewe mwenyewe.
Badala ya kujilinganisha na wenzako ambao wanaonekana wamefanikiwa kuliko wewe na kuanza kujisikia vibaya hebu anza kujilinganisha na wewe mwenyewe. Jiulize hicho unachofanya kwenye maisha yako je unakifurahia? Kumbuka ni vigumu sana kufanikiwa kama unafanya kitu ambacho hukipendi
No comments:
Post a Comment