Miaka ya hivi karibuni dhana inayohusu ujasiriamali imeenea kwa kasi kubwa sana miongoni mwa wana jamii. Kwa sasa kila kona tunasikia ujasiriamali, makanisani , mitaani, vyuoni na katika mikutano ya kisiasa kunahubiriwa ujasiriamali. Hata hivyo kuna kibwagizo kinajirudia kila zinapotajwa changamoto za ujasiriamali; ukosefu wa mitaji!. Dhana ya ujasiriamali imepata kushika kasi kutokana na nchi yetu kujikuta inajisalimisha katika mfumo wa kibepari pasipo kupenda wala kutoa taarifa. Utandawazi umeyasababishia mataifa masikini kama Tanzania kurukia ubepari bila kuagana na...
nyonga zao.
Nyonga ninazomaanisha hapa ni mifumo ya kiuchumi iliyokuwepo nap engine
iliyobuniwa na wazalendo wa mataifa husika; Tanzania tukiwa na ujamaa wetu
ulioasisiwa na mwalimu Julius Nyerere.
Inafaa sana
watanzania wote kufahamu kuwa maisha ni magumu. Na ugumu wa maisha haujaanza
jana wala miaka ya karibuni, bali tangu uwepo wa dunia hii maisha ni magumu.
Wengi huwa hawataki kuukubali ukweli huu ‘kama ulivyo’.
Ndio maana
utawasikia wakihuzuniaka, kung’ung’unika na kulalamika, kana kwamba waliambiwa
maisha ni rahisi. Saa unapoukubali ukweli ya kuwa maisha ni magumu, ndio wakati
ambao maisha hayawi magumu tena! Ndio! Kwa sababu ukijua maisha ni magumu ni
lazima utaishi kwa nidhamu kubwa, na nidhamu ndio msingi namba moja wa kutatua
matatizo yote katika maisha.
Ukiwa na
nidhamu kidogo utatatua matatizo machache, na ukiwa na nidhamu nyingi utatatua
matatizo mengi! Nidhamu inahusisha kufanya kazi kwa bidii, kuwapenda na
kuwafikiria wengine, kuheshimu sheria za nchi na kila namna ya jema
unalolijua.
Ukiona
unalalamika kuwa maisha ni magumu, rejea katika fikra zako, huenda bado
hakujafanyika mapinduzi! Ukiona unaukubali ukweli ya kuwa maisha ni magumu na
wakati huo huo huna nidhamu ama una nidhamu chache, basi ujue kuwa hujaukubali
ukweli wote wa maisha kuwa ni magumu, !
Ujasiriamali
unawagusa watu wa kada na umri mbalimbali, vijana wazee na hata watoto. Kwa kuwa
kundi la vijana [wasomi na wasio wasomi] ndio linaloongoza sana kwa kutegemewa
kwa uzalishaji nitaongelea hilo. Ujasiriamali kwa ujumla ni dhana ambayo ili
kukubalika kikamilifu kunahitajika mapinduzi makubwa sana ya fikra kwa vijana
kuliko elimu ya kawaida. Fikra za kuwatazama wajasiriamali waliofanikiwa na
kutoa visingizio kuhusu mafanikio yao ni fikra zenye matege na ukilema na hizo
kamwe haziwezi kutufanya tukafanikisha kujikwamua kiuchumi.
Vijana ambao
hawana elimu wanalalamika kuwa hawana elimu ndio maana maisha yao ni magumu ama
yanasumbua, nao vijana ambao wanaelimu katika fani na viwango mbalimbali
wanalalamika kuwa ajira hamna. Unapogusia suala la ujasiriamali katika kundi
hili la vijana wenye elimu, utakisikia kilio ambacho kimekuwa kama wimbo sasa
nacho ni “ukosefu wa mitaji”. Kwa ufupi ni kuwa vijana wenye elimu wanalia
kutokana na ugumu wa maisha na vile vile vijana wasio na elimu wanalia. Wasio na
elimu wanawatamani wenye elimu, na wenye elimu wanaitamani mitaji.
Kutokana na
hali hii utagundua kuwa tatizo linaliwakabili vijana wengi wa Tanzania katika
kujikwamua kiuchumi sio mitaji wala ukosefu wa elimu bali kuna tatizo la kifikra
hapa. Ili kijana aweze kufanikiwa kubuni na kuanzisha mradi anatakiwa aamini
kuwa kujiajiri kuna tija kubwa sawa sawa na kuajiriwa. Kwa sababu ni mara chache
sana mtu anaweza kuwa tajiri kwa kutegemea mshahara wake!
Kwa bahati
mbaya katika jamii kuna utamaduni uliojengeka sana katika jamii zetu wa kuamini
sana kuajiriwa. Hata familia nyingi zinaposomesha watoto wao zinawasisitiza
wasome kwa bidii ili wafaulu na kupata kazi zenye mishahara mikubwa. Utamaduni
huu umefifisha hamasa na moyo wa kupenda kujiajiri miongoni mwa vijana wetu hasa
waliopo katika mifumo ya kielimu..
Hebu
tumtafakari kijana anayesema kuwa amekosa mtaji ndio maana ni masikini. Ni
dhahiri kuwa wengi wa vijana mara kwa mara huwa wanabahatika kupata, shilingi
elfu ishirini mifukoni mwao. Kijana akitumia ubunifu, kwa mfano anaweza kununua
kuku wawili wa kienyejji wa kufugwa, kila mmoja shilingi elfu saba, jumla wawili
ni elfu kumi na nne.
Hawa
wakifugwa kwa miezi mine wanaweza kutotoa kuku kumi. Baada ya mwaka mmoja kuku
wanaweza kufikia sitini! Kuku sitini ukiwauza kwa shilingi elfu saba kila mmoja
anakuwa na zaidi ya laki nne. Tayari huyu anakuwa ameanza safari ya kujikwamua
na umasikini!
Vijana wa
Tanzania ambao wanapambana na ugumu wa maisha wanahitaji sana kupokea semina,
shuhuda na uzoefu kutoka kwa wajasiriamali wa kitanzania ambao wamefanikiwa.
Kama semina, warsha na makongamano yatakuwa yakitumia dhana pekee za vitabuni
tutarudi kule kule katika mfumo tegemezi, ambao unaonekana sio halisi bali ni wa
kujibia mitihani. Tunawahitaji wajasiriamali vijana kuandika vitabu vinavyoeleza
namna walivyofanikiwa ili kutia hamasa na kubadilisha fikra za vijana wengine
ambao wanasua sua kujikita katika ujasiriamali kwa visingizio vya kukosa elimu
na kukosa mitaji.
Ujasiriamali
unahusisha kujenga fikra madhubuti za kujitegemea na kutegemewa. Kwanza ni kuwa
akili ya mtu inapanuka na kuwaza zaidi na zaidi kutegemea na mahitaji yaliyopo
katika fikra. Ukiwaza kupata fedha kidogo ya kujikimu ubunifu wa akili yako
utajikita katika upatikanaji wa fedha hiyo kidogo! Ukiwaza kuwa na fedha nyingi
akili yako inapanuka kuwaza namna ya kupata fedha nyingi. Lengo langu hapa si
kusisitiza vijana kuwa na fedha nyingi, isipokuwa ni kuweka hamasa kwa vijana
kuhusu ujasiriamali na namna ya kujikwamua kiuchumi.
Ni vema
vijana wote wafahamu ya kuwa “fedha ni mawazo”. Kama fedha ni mawazo basi
kujikwamua kiuchumi ni mawazo pia. Kama ni suala la kuwaza, kwa nini asiye na
elimu asiwaze? Kama ujasiriamali unaanza na mawazo, kwa nini wenye elimu walilie
mitaji? Sikatai kuwa mitaji ni suala la msingi katika ujasiriamali, lakini
ifahamike kuwa uthubutu wa kuanza na kujaribu wazo hata kwa sehemu ndogo ndio
msingi wa mafanikio ya mjasiriamali yeyote.
Nchi ya
Tanzania ina ajira na fursa nyingi sana za kiuchumi za kumtosha hata mtoto
atakayezaliwa kesho! Sioni sababu ya muhitimu wa darasa la saba kukosa ajira,
kwa nini muhitimu wa kidato cha nne na sita wakose kitu cha kufanya chenye
kuwakwamua kiuchumi katika nchi tajiri kama Tanzania? Kwa wale ambao ni wahitimu
wa vyuo vya kati na vya elimu ya juu sioni haja ya kuwaandikia kwa sababu
inatosha sana kwao kutengeneza ajira kwa wengine.
Tatizo
jingine linalowasibu vijana wengi wa Tanzania hata wanashindwa kupoka (Seizing)
fursa za kijasiriamali na fikra potofu za kutaka kuanza na mafanikio. Kama ni
kijana msomi anawaza kuanza na kampuni lenye mtaji wa mamilioni. Yatatoka wapi
mamilioni bila kuanza na kudogo? Kwa wale ambao hawana elimu kubwa wengi wamevia
kimawazo kwa kuota kuokota fedha ama kuokota elimu.
Kama ulikosa
elimu haupaswi kulalamika wala kung’ung’unika kwa sababu huko ni kupoteza muda
bado unayo nafasi kubwa sana ya kufanikiwa. Fikra za kupata vya bure bila
kuhangaika ndio zinapelekea watanzania wengi kujiingiza katika michezo mingi ya
‘kibahati nasibu’ kwa matarajio kuwa watatoka! Cha ajabu ni kuwa michezo mingi
inayohusu bahati nasibu ama mingineyo inawapotezea fedha badala ya kuwasaidia,
hapa yanahitajika mapinduzi ya kifikra.
Maisha bora
na ya uhakika kwa vijana yanawezekana sana ikiwa kutafanyika mageuzi makubwa
katika sekta binafsi, ujasiriamali. Na ili ujasiriamali ufanikiwe na kufanywa na
vijana kwa uhakika ni lazima vijana wote wakubali kufanya mapinduzi ya fikra zao
za kitegemezi. Tukisema ujasiriamali hatumaanishi ujasiriamali wa kujikwamua
wewe kijana peke yako, bali tunagusa pia katika utanuzi wa fikra za kuanzisha
makampuni, huduma na bidhaa mbalimbali zenye ubunifu mpya kwa kuvitumia vipaji
kikamilifu
Watanzania
tunahitaji ushindi wa kiujasiriamali!
No comments:
Post a Comment