Wakiwa na majeruhi ya kipigo walichopata wiki mbili zilizopita kutoka kwa mahasimu wao Manchester United – Liverpool leo walisafiri mpaka jijini London kwenda kupambana na kuweka hai matumaini ya kuingia Top 4 kwa kucheza dhidi ya Arsenal.
Hata hivyo matumaini yao ya kuingia kwenye Top 4 yamezidi kupotea baada ya kukubali kupewa kibano cha magoli 4-1 kutoka kwa Arsenal.
Mpaka dakika 45 za kwanza zinamalizika ubao wa matokeo ulikuwa unasomeka Arsenal 3-0 Liverpool – Hector Bellarin, Mesut Ozil na Alexis Sanchez wakiwa wafungaji wa magoli hayo.
Kipindi cha pili Liverpool walianza kwa kumuingiza Daniel Sturridge na kufanikiwa kupata goli moja baada ya Raheem Sterling kufanyiwa madhambi na Bellarin kisha Henderson akafunga mkwaju wa penati.
Huku dakika zikiwa zinayoyoma mwanasoka bora wa mwezi March katika EPL – Oliver Giroud alifunga goli zuri kabisa na kushindilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la Liverpool leo hii.
Kwa matokeo hayo Arsenal wamepanda mpaka nafasi ya pili kwenye ligi.
Ligi kuu ya England imeendelea tena jioni ya leo baada ya kupisha mechi za kimataifa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Manchester United baada ya kupata matokeo ya ushindi dhidi ya wapinzani wao wa jadi Liverpool wiki mbili zilizopita – leo hii walikuwa katika dimba lap la nyumbani kucheza dhidi ya Aston Villa.
Villa waliingia Old Trafford wakiwa na kumbukumbu ya kupata sare ya 1-1 dhidi ya United katika raundi ya kwanza ya EPL – lakini leo hii hali ilikuwa tofauti wakicheza na United ambayo ipo katika kiwango cha juu.
Matokeo ya mchezo huo ni ushindi wa 3-1 kwa vijana wa Louis Van Gaal.
Magoli ya Ander Hererra aliyefunga mawili na Wayne Rooney aliyefunga moja yalitosha kuipeleka United mpaka nafasi ya 3 katika msimu wa ligi mbele ya Man City ambao watakipiga na Crystal Palace jumatatu usiku.
Man U itakairibisha City Old Trafford wikiendi ijayo katika mchezo wa raundi ya pili ya EPL.
Wakati Arsenal na Manchester United wakizidi kuisogelea katika kilele cha uongozi wa ligi kuu ya England – Chelsea leo imeikaribisha Stoke katika uwanja wa Stamford Bridge katika harakati za kujihakikishia nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Mchezo huo uliomalizika hivi punde – umeshuhudia vijana wa Jose Mourinho wakiongeza pengo la pointi dhidi ya wapinzani wao City, Arsenal na Man United, baada ya kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya Stoke.
Goli la Eden Hazard kupitia mkwaju wa penati katika dakika ya 39, liliwapa Chelsea uongozi wa dakika 5 – kabla ya Charlie Adam kufunga goli zuri kutoka katikati ya uwanja na kuisawazishia Stoke City.
Kipindi cha pili Chelsea walipata pigo baada ya Diego Costa kudumu uwanjani kwa dakika 10 na kuumia – nafasi yake ilichukuliwa na Didier Drogba.
Loic Remy aliifungia Chelsea goli la pili na ushindi baada ya Hazard kufanya kazi kwa kupora mpira uliorushwa vibaya na golikipa Begovic.
Chelsea wamefikisha pointi 70 huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi – Arsenal wanawafuatia wakiwa na pointi 64.
MSIMAMO WA LIGI UPO KAMA HIVI:
CHEKI VIDEO HAPO CHINI:
No comments:
Post a Comment