Breaking News
recent

MFUMO MBOVU WA ELIMU NA TATIZO LA AJIRA TANZANIA





Kwa miaka michache iliyopita tatizo la ajira limeanza kushika kasi Tanzania na kwa miaka michache ijayo litakuwa tatizo sugu kama hatua za makusudi hazitochukuliwa. Tatizo hili kila mtu analiona na viongozi mbalimbali wamekuwa wakilizungumzia. Ni kweli tatizo lipo na linaonekana, ila ni kweli kila anaeliona anafahamu chanzo halisi cha tatizo hilo? Na je njia na ushauri unaotolewa na viongozi mbalimbali kuhusiana na tatizo la ajira zinaweza kulimaliza ama kulipunguza tatizo? Wahitimu waliokosa ajira wanashauriwa kujiajiri, je tuna uhakika wameandaliwa kujiajiri?
Lazima tujue kiini cha tatizo ili tuweze kukabiliana nalo sawa sawa. Chanzo kikubwa cha tatizo la ajira ni mfumo wa elimu. Tukiangalia historia ya elimu Tanzania, tulirithi mfumo wa elimu kutoka kwa wakoloni na mpaka sasa tunatumia mfumo huo ukiwa umefanyiwa marekebisho ya hapa na pale. Lengo kubwa la elimu ya kikoloni lilikuwa kuandaa wafanyakazi na wasaidizi wa wakoloni. Walilenga kupata wafanyakazi wachache wenye elimu za juu ili kuwa wasimamizi na wafanyakazi wengine wenye elimu za kati kuwa wasaidizi. Walilenga tupata wafanyakazi wa serikalini, viwandani na watoa huduma kama walimu na madaktari. Leo ni miaka zaidi ya hamsini imepita tangu tupate uhuru na bado elimu yetu ipo kwenye mlengo huo huo, kuandaa wafanyakazi. Sio vibaya elimu kuandaa wafanyakazi, tatizo ni kazi zipo? Unaandaa wafanyakazi una viwanda? Una uwezo wa kuwaajiri? Sekta binafsi zina uwezo kiasi gani wa kuajiri? Ukiangalia kwa makini uwezo wa serikali na sekta binafsi wa kuajiri ni mdogo ukilinganisha na idadi ya wafanyakazi wanaozalishwa kila mwaka. Kwa kuwa uwezo wa kuajiri ni mdogo ushauri unaotolewa kwa wahitimu ni waende wakajiajiri. Ni ushauri mzuri ila wataanzia wapi kujiajiri? Mfumo mzima wa elimu kuanzia darasa la kwanza mpaka chuo kikuu unamfundisha mwanafunzi kuajiriwa, nyumbani wazazi na jamii wanamsisitiza mtoto asome kwa bidii afaulu vizuri ili apate ajira nzuri. Hata mwalimu anaemfundisha anamwambia “ukienda kazini utafanya hivi.” Kwa mazingira yote haya unakuja kumpa jibu rahisi kwamba aende akajiajiri. Ni ngumu sana kwa mtu huyu kufunguka haraka kwa sababu mfumo mzima wa elimu na maisha umeshamharibu. Inabidi kwanza abadili mtazamo ndipo aweze kukabiliana na mazingira hayo mapya kwake, kitu ambacho kinawaumiza na kuwavuruga wengi kisaikolojia.
Kwa maoni yangu ni muhimu kubadili mfumo wa elimu, ni vyema tukaangalia ni nini changamoto zetu kama taifa na kuangalia mfumo mzuri wa elimu utaoweza kututoa hapa tulipo. Tuwe na mfumo ambao mwanafunzi aliemaliza kidato cha nne akapata daraja sifuri ana kitu cha kufanya na sio anaishia kuonekana ni mjinga ama amefeli. Hiyo ni kitaifa na kiserikali na nina uhakika mengi yameandikwa na kushauriwa ila utekelezaji ndio tatizo kubwa. Kwa kuwa wanaotakiwa kutekeleza hawafanyi hivyo haiwezi kuwa sababu ya mtu mmoja mmoja kushindwa kubadili hili. Kila mtu achukue hatua, wafundishe watoto wako, washwawishi ndugu na jamaa zako kubadili mtizamo. Ushauri mkubwa ninaoutoa hapa kwa wanafunzi walioko shuleni na vyuoni ni wafikirie nje ya boksi, hayo unayofundishwa chuoni anza kufikiria unaweza kuyatumia vipi kujiajiri, soma maandiko na vitabu mbalimbali vinavyoweza kukusaidia kimaisha na kiuchumi. Usisubiri ukifika mtaani ndio uanze kuhangaika, jua kabisa unasoma ila huku mtaani ajira hakuna. Angalia wenzako waliokutangulia wengi bado wako mtaani wakihangaika kutafuta ajira mwaka mzima mpaka miwili. Ukiwa umejiandaa inakuwa afadhali kuliko ukiwa hujajiandaa kabisa.
Huwezi kubadili maisha yako kama hutobadili mtazamo/fikra zako
NINI MAONI YAKO?
 
Posted by BonifaceJr
Unknown

Unknown

No comments:

Powered by Blogger.